Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

25th APRIL 2024

 




KUJAZWA NEEMA NA KUTANGAZA NENO LA MUNGU KWA MAPENDO



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Aprili 25, 2024 
------------------------------------------------
ALHAMISI, JUMA LA 4 LA PASAKA
SIKUKUU YA MT. MARKO, MWINJILI

Somo la 1: 1 Pet 5:5-14 Somo linaongelea kuhusu Marko, ambaye Patro alimchukua kama mtoto wake. 

Wimbo wa Katikati : Zab 89: 2-3, 6-7, 16-17 Maisha yote midomo yangu itatangaza ukweli wako. 

Injili: Mk 16: 15-20 Yesu anawambia wale kumi na mmoja waende ulimwenguni kote; wakahubiri kwa mataifa yote. 
------------------------------------------------

KUJAZWA NEEMA NA KUTANGAZA NENO LA MUNGU KWA MAPENDO 

Leo kanisa linasheherekea sikukuu ya Mt. Marko Mwinjili. Yohane Marko anatokea katika kitabu cha Matendo ya mitume (Mdo 12:12), na mara nyingi ametajwa katika katika barua za Petro na Paulo. Katika barua fupi ya filemoni Marko ananukuliwa kama rafiki wa karibu wa Paulo…’.. Marko Mwanangu”. Kuna mapokeo pia kwamba Marko alikuwa ni mwanzilishi wa kanisa la Alexandria, kaskazini mwa Misri. Mwandishi wa Injili ya Pili pia inasemekana pia ya Marko. Mapokeo yanasema pia wakristo wa Roma alimuomba Marko aandike maneno ya Petro. Na Injili inaoneakana kuandikwa kama utume wa Yesu kama alivyo uona Petro na hivyo Marko kuandika. Inasemekana ni Injili ya kwanza kuandikwa, na Mathayo na Luka inaonekana kupata kutoka kwake. Injili yake imejaa matendo ya Yesu, ambapo Yesu anafundisha zaidi yale anayotenda kuliko yale anayosema. 

Katika Injili ya leo Yesu anawapa mamlaka kutangaza Injili kwa kila kiumbe na kuna ahadi kwamba waamini watakuwa na uwezo wakutenda makuu-kutoa pepo, kunena kwa lugha, kukingwa na mabaya na kuponya wagonjwa. Na mwishoni somo linaonekana kuwa na maelezo kidogo kuhusu kupaa ambapo Bwana wetu alikuwa akirudi kwa baba yake, na kukaa mkono wa kuume wa Mungu. Marko anaelezea changamoto za wafuasi wa Kristo na katika kutimiza hali yao ya umisionari na kuanzisha Ufalme ambao mapenzi ya Mungu yatatendwa duniani. 

“Enendeni ulimwenguni mote mkahubiri Injili kwa kila kiumbe” (Mk 16:15). Amri iliyo ya kawaida kabisa. Na wimbo wa katikati unasema hivi “nitaimba daima sifa zako, ee Bwana, muda wote nitatangaza uaminifu wako…ni nani aliye kama Bwana.” Yesu aliwatuma wanafunzi wake ambao walikuwa watu wakawaida lakini wakiwa wamejaa nguvu ya ajabu ili kutangaza Injili yake na kuikomboa dunia. Cha muhimu haikuwa msingi wa wafuasi kuhubiri bali msingi wa kutegemea neema yake inayofanya kazi ndani yao na hivyo kwa namna tulivyo wawazi kwa neema ya Mungu, ndivyo neema yake inavyotiririka ndani yetu. Uwazi wetu kwa Mungu utasababisha matunda makubwa zaidi ya jinsi tusivyoweza kutegemea. 

Sala: Yesu, nisaidie mimi niweze kuwa wazi kwa neema yako. Tunakuomba utupe neema tuweze kumuiga Mt. Marko Mwinjili katika roho ya kutangaza Ufalme wako. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, APRILI 25, 2024



MASOMO YA MISA, APRILI 25, 2024
JUMA LA 4 LA PASAKA, ALHAMISI
SIKUKUU YA MTAKATIFU MARKO, MWINJILI


SOMO 1 
1 Pet 5: 5-14

Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika ¡mani, mkijua ya kuwa mateso yale yaie yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika «risto, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina. 

Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu. Salimianeni kwa busu la upendo. Amani na iwe kwenu — nyote, mlio katika Kristo. Amina.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 89: 1-2, 5-6, 15-16

(K) Fadhili zako nitaziimba milele, Ee Bwana 
au: Alleluya

Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, fadhili zitajengwa milele;
katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. (K)

Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako,
uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana?
Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa malaika? (K)

Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,
Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,
Na kwa haki yako hutukuzwa. (K)

SHANGILIO 
1 Kor. 1:23-24

Aleluya, aleluya,
Sisi tunamhubiri Kristu, aliyesulibiwa, ni nguvu na hekima ya Mungu.
Aleluya.

INJILI 
Mk 16: 15-20

Yesu aliwaambia wale Kumi na mmoja, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hatawakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na ulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristu. 



Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

YESU, MWANGA KWA ULIMWENGU!



“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumatano, Aprili 24, 2024. 
Juma la 4 la Pasaka


Mdo 12:24-13:5;
Zab 67:2-3,5-6,8 (K. 4);
Yn 12:44-50.


YESU, MWANGA KWA ULIMWENGU!


Kumfahamu Yesu ni kumfahamu Baba pia. Ukweli ni kwamba uwepo wa Baba umefunikwa kama Umungu wa Kristo ulivyo funikwa. Ingawaje hatuna uzoefu wa kumuona Yesu akitembea kama wale wafuasi wa kwanza walivyo muona, tunakutana na ukweli huo huo katika Ekaristi Takatifu. Wakati tunapo ingia kanisani na kupiga goti kuelekea Tabernakulo, ni vizuri kuwa na uelewa na kufahamu kuwa tupo mbele ya uwepo wa Mungu Mwana. Na kwa njia hiyo tupo pia mbele ya uwepo wa Mungu Baba! Uwepo wao ni wazi na hakika. Ni kwasabau tu wamefichwa kutoka katika milango yetu mitano ya fahamu. 

Katika Injili, Yesu anakuja kama nuru ili tusiwe tena kwenye giza. Anakuja kwa lengo hili: tumuamini yeye na kuwa na ukweli na uzima. Zaburi ya 27 mstari wa 1, unasema “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu”. Kama ilivyo mwanga wa kawaida hufunua kile kilicho fichwa kwanye giza, vivyo hivyo Neno la Mungu huleta nuru ili tuweze kutambuaa ukweli ulio fichika ndani ya Ufalme wa Mungu. Kama nuru, huleta furaha na uzima kwa wengine. Inafanya mbegu ya imani ikue ndani yetu, ili tuweze kushiriki furaha ya Mungu na uzima na wengine. Sisi mara nyingi tunachagua kubaki kaburini kama Mafarisayo bila kufufuka. Lakini Yesu ni mlango wa uzima wa milele. Kwani Yesu ni uzima na ufufuo na wote wale wanao mwamini watakuwa na uzima wa milele. 

Sala: Bwana, nisaidie niweze kukuelewa wewe na kukupenda wewe na katika uhusiano huo niweze kumfahamu na kumpenda Baba na Roho Mtakatifu. Bwana, ninaomba wewe uwe mwanga ambapo kwa njia yako niweze kukuona wewe na ulimwengu. Yesu nakuamini wewe. Amina.


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, APRILI 24, 2024



MASOMO YA MISA, APRILI 24, 2024
JUMATANO, JUMA LA 4 LA PASAKA


SOMO 1
Mdo. 12:24-13:5

Siku zile, Neno la Bwana likazidi na kuenea. Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohane aitwaye Marko.

Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.

Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami waklihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 67:1-2, 4, 5, 7 (K) 3

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru. au Aleluya.

Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)

Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)


SHANGILIO
Yn. 10:14

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema,
Nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.


INJILI
Yn. 12:44-50

Siku ile Yesu alipaza sauti, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeyey anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

24th APRIL 2024



 

23rd APRIL 2024

 




22nd APRIL 2024

 



KUMFUATA MCHUNGAJI MWEMA!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumatatu, Aprili, 22, 2024
Juma la 4 la Pasaka

Mdo 11:1-18;
Zab 42:2-3,43:3-4 (K. 42:3);
Yn 10:11-18.


KUMFUATA MCHUNGAJI MWEMA!

Sehemu ya Injili ya mchungaji mwema inatupa mambo manne kuhusu Yesu. Kwanza kabisa Yesu kwa kuwa Neno wa Mungu mwenyewe, sio tu mchungaji bali yeye mwenyewe ni chakula-malisho ya kweli ambaye hutoa uzima kwa wingi. Anatupa uzima kwa kujitoa mwenyewe, kwani yeye ni uzima (Yn 1: 4). Pili, huyu Mchungaji mwema anatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake (Yn 10: 11). Msalaba upo katikati ya maelezo ya Mchungaji mwema. Na unaoneshwa sio kama kitendo cha vita kinacho mshtukiza Yesu bila kujua na kumshambulia kutoka nje, bali ni kama zawadi huru kutoka kwake. “Nayatoa maisha yangu, ili niya twae tena. Hakuna awezaye kuyatwaa kutoka kwangu, bali ninayatoa kwa hiari yangu mwenyewe”.

Tatu, kondoo ni wake katika hali ya kufahamiana na mchungaji, na hali hii ya kufahamiana ni hali ya kukubali kutoka ndani. Ina maanisha hali ya kuwa wake katika hali ya ndani ambayo ni zaidi ya ile hali ya kuwa na vitu vya kawaida. Na mwisho Kabisa, Mungu ndiye mchungaji ambaye anawaunganisha tena Waisraeli waliogawanyika na kutawanyika na kuwafanya watu wamoja kwani sio mataifa mawili tena (Ez 37: 15-17, 21). Hili ndilo la Muhimu kwa wayahudi walipo mpinga Petro kwa kutembelea nyumba ya Kornelio kama inavyo oneshwa katika somo la kwanza. 

Sisi nasi tunaalikwa kwenye utume sisi kama wachungaji wa Kristo tunapaswa kuziokoa roho kwa ajili ya Mungu kwa kulijenga na kulifanya kanisa la Mungu kuwa moja. Je, tupo tayari kuchukua jukumu hili na kukumbana na changamoto? 

Yesu, Mchungaji Mwema, anatuita sisi "kondoo," kwamba sisi ni dhaifu na wanyonge. Bila yeye, hatuwezi kufanya kitu (Yn 15: 5). Mchungaji Mwema atosha, Yeye atawaongoza kwenye malisho ya majani mabichi (Zab 23: 2). Jambo pekee linalohitajika kutoka kwetu sisi kondoo, ni kusikia sauti yake daima na kuifuata. Sisi sote kama kondoo lazima tuikimbie sauti ya yule muovu (Shetani). Sauti ya Yesu inahitaji kujitoa kweli, kujikana nafsi na kuacha yote, kubeba misalaba yetu, tofauti na sauti nyingine za ulimwengu huu zinazo onekana kuwa tamu na rahisi kuzifuata lakini mwisho wake kuangamia milele. Kusikiliza sauti ya Yesu ni katika Sala na Tafakari juu ya Biblia, kuwasikiliza ndugu zetu katika hali mbali mbali na mengine yanayo tujenga kiroho. Kusikiliza huja kwa Neno la Kristo (Rum 10:17). Tumuombe Mungu atusaidie kuisikia sauti ya Yesu ndani ya sauti nyingi za ulimwengu huu. 

Sala: Bwana, nisaidie niweze kutambua na kufuata sauti yako ya upole siku zote za maisha yangu. Ninaomba sauti hiyo iweze kushinda sauti zote zinazo shindana na utulivu wangu kwako. Ninakuchagua wewe, Bwana mpendwa kama mchungaji wa kuniongoza. Yesu nakuamini wewe. Amina.

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, APRILI 22, 2024


MASOMO YA MISA, APRILI 22, 2024
JUMA LA 4 LA PASAKA, JUMATATU

SOMO 1
Mdo 11:1-18

Siku zile, mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.

Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wan chi wenye miguu mine, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.

Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishwi. Ndugu hawa sita nao wakaenda nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.

Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukuia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohane alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatiza kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu?

Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba lilitalo uzima.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 42:1-2, 43:2-3 (K) 42:2

(K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai.
Au Aleluya.

Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji,
Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, ee Mungu. (K)

Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
Lini nitakapoikuja nionekane mbele za Mungu? (K)

Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze, 
Zinifikishe kwenye mlima wako
mtakatifu na hata maskani yako. (K)

Hivyo nitakwenda madhabahuni mwa Mungu,
Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu;
Nitakusifu kwa kinubi, ee Mungu, Mungu wangu. (K)


SHANGILIO
Ufu. 1:5

Aleluya, aleluya,
Ee Kristo, yu shahidi aliye mwaminifu mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.


INJILI
Yn. 10:1-10

Yesu aliwaambia Wayahudi: Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo wake wote, huwatangulia; na awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.

Mithali hiyo Yesu aliwaambia; lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.

Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo. 

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.