Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

2nd NOVEMBER 2025


 

MASOMO YA MISA NOVEMBA 2, 2025

 


MASOMO YA MISA NOVEMBA 2, 2025
JUMAPILI, JUMA LA 31 LA MWAKA WA KANISA

KUWAKUMBUKA WAAMINI MAREHEMU WOTE

(Masomo haya na zaburi yamechaguliwa kutoka masomo mengine mengi ya siku ya leo.)

SOMO 1
Isa 25: 6-9

Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana. Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema,Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidiye; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23 (K) 1 au 4


(K. 1) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. (au)
(K. 4) Nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; Kwa maana wewe upo pamoja nami

Bwana ndiye mchungaji wangu, 
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza.
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)

Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jjina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yangu vyanifariji. (K)

Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)

Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)


SOMO 2
Rum 5:5-11

Tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikuwa kwa ajili yetu, tulipokwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu 


SHANGILIO
Ufu. 14:13

Aleluya, aleluya,
Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa! Wapate kupumzika baada ya taabu zao, kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.
Aleluya.


INJILI
Mk 15: 33-39, 16: 1-6.

Ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona
umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni; na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini. Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.

Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza.

Wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakaye-vingirisliia lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata waalipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno. Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu. Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.     

MIMI NI UFUFUO NA UZIMA!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumapili, Novemba 2, 2025
Juma la 31 la Mwaka wa Kanisa

KUWAKUMBUKA MAREHEMU WOTE

Is 29:6-9;
Zab 23;
Rom 5:5-11;
Mk 15: 33-39, 16: 1-6.


MIMI NI UFUFUO NA UZIMA!


Leo Kanisa Katoliki linawaombea watoto wake, ambao katika siku ya kufa, japo walitamani utukufu usio na mwisho Mbinguni, hawakuwa wamejiandaa vyema kuingia katika furaha hiyo na pia hawastahili kwenda motoni. Hawa ni roho zilizoko twaharani- ambao wanatakaswa ili waweze kuurithi ufalme wa mbinguni. Lakini pia sisi tujifunze kitu kwamba kila mmoja wetu amesogea siku moja kuelekea kifo. Ni njia yetu wote.

Sala kwa ajli ya marehemu zilianza na Wakristo wa kwanza, mwanzoni kabisa, kuwaombea mashahidi wa kwanza. Walifanya hivyo kumshukuru Mungu mwenyenzi kwa ajili ya mashahidi wa kwanza kwa ujasiri wao, na zaidi sana kwa Imani yao. Walifanya hivyo kwasababu walitambua kifungo kisichoweza kuvunjwa kinacho tuunganisha sisi ndani ya Kristo, walio hao na waliokufa pia. Kifo hakiwezi kuvunja na kutenga familia ya Kristo, hakiwezi kuharibu umoja na muunganiko wetu tunao shiriki katika Kristo sisi zote kama tupo hapa duniani au tumeenda katika maisha yajayo.

Kuwaombea wafu ina msingi wake katika maandiko matakatifu “na hivyo (Yuda Wamakabayo) akafanya maombi kwa ajili ya kuwaombea wale waliokufa, ili wasamehewe dhambi zao” (2 Mak 12:46). Kuanzia mwanzoni, Kanisa limeheshimu kuwakumbuka marehemu na kutolea sala kwa ajili yao, na juu ya yote sadaka ya Ekaristi, ili waoshwe, waweze kupata heri ya mwanga wa Mungu. Kanisa pia linahimiza kutolea sadaka, rehema, na kazi za toba kwa niaba ya marehemu (KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI, 1032).

Lakini hata tungekuwa na ujasiri namna ghani na hata tukipokea ukweli katika hali ya chanya, siku ya kuiacha dunia hii haieleweki na ni lazima, kwasababu kunakuwepo na utengano wa mwili na roho. Hivyo Kanisa linatuhimiza kila mara kujiandaa wenyewe kila mara kwa saa ya kufa kwetu. 

Sala: Mungu mwenye nguvu na huruma, umefanya kifo kiwe mlango wakuingia uzima wa milele. Uwatazame kwa huruma ndugu zetu marehemu, wafanye wawe pamoja na Mwanao kwa mateso na kifo, ili, wakiwa wamefunikwa na damu ya Kristo, waweze kuja mbele zako wakiwa huru kutoka katika dhambi. Amina.


Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

WATAKATIFU: WITO WA WATU WOTE WA KUWA WATAKATIFU!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi, Novemba 1, 2025
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Sherehe ya Watakatifu Wote

Uf 7:2-4, 9-14;
Zab 23:1-6;
1 Yn 3:1-3;
Mt 5:1-12


WATAKATIFU: WITO WA WATU WOTE WA KUWA WATAKATIFU!


Watakatifu ni wale walio jitahidi kuishi hapa duniani kadiri ya thamani ya Injili. Hata baada ya kifo chao wanaendelea kuwa mfano na mashuhuda wa Injili kwa wale waliobaki dunaini. Wakiwa wameumbwa wakiwa na mwili na damu kama sisi walitamani kupata utakatifu. Hawa ni wale waliopata moyo kutoka kwa watakatifu wengine wakisema “kama yeye amekuwa mtakatifu kwanini mimi nisiwe?” Watakatifu mbinguni wana bahati ya kuwa mbele za Mungu daima. Walio wengi wakiwa bado hapa duniani walifurahia kuwa ndani ya Mungu daima wakiwa hapa duaniani. Mginguni ni pale alipo Mungu, na Mungu yupo ndani ya mioyo yetu, kwahiyo walikuwa na Mungu daima mbinguni. Watakatifu waliishi wakilijua hili na wakajikuta wakiwa katika furaha ya Mungu daima.

Injili ya Leo inatualika kufuata zile heri kama njia ya kuelekea kupata Utakatifu. Sisi ni nani tuishi maisha ya utakatifu? Mt. Augustino alijikuta akipata ugumu wakuishi heri hizi, lakini alisoma maisha ya watakatifu na akasema, “ Kama hawa watu wakawaida waume kwa wake waliweza, kwanini mimi nisiweze?”

Sala: Bwana, umetuita kuwa wakamilifu kama Baba yetu wa Mbinguni. Tuwekee ndani yetu hamu ya kukufurahisha wewe kwa kila kitu na utufundishe njia ya ukamilifu. Amina



Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 1, 2025



MASOMO YA MISA, NOVEMBA 1, 2025
JUMAMOSI, JUMA LA 30 LA MWAKA WA KANISA
SHEREHE YA WATAKATIFU WOTE

SOMO 1
Ufu. 7:2-4,9-14

Mimi Yohane, niliona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari, akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao. Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu.

Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-kondoo.

Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu, wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa aliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Nao wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 24:1-6 (K) 6

(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. (K)

Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)

Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)


SOMO 2
1 Yoh. 3:1-3

Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa; kama yeye alivyo mtakatifu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu


SHANGILIO
Mt. 11:28

Aleuya, aleluya.
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha, asema Bwana.
Aleluya.


INJILI
Mt. 5:1-12

Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjua; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,

Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania. These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA OKTOBA 31, 2025

 



MASOMO YA MISA OKTOBA 31, 2025
IJUMAA, JUMA LA 30 LA MWAKA
_____________

SOMO 1
Rum. 9:1-5

Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina. 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 147:12-15, 19-20 (K) 12

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)

Ndiye afanyaye Amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K)

Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
Aleluya. (K)


SHANGILIO
Zab. 119:34

Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.


INJILI
Lk. 14:1-6

Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponywa siku ya sabato, ama sivyo? Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.

_____________

Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

31st OCTOBER 2025


 


KUWA NA HURUMA



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI” 
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Oktoba 31, 2025
Juma la 30 la Mwaka

Rom 9: 1-5;
Zab 147: 12-15, 19-20 (K) 12; 
Lk 14: 1-6.


KUWA NA HURUMA


Leo Yesu anwauliza Mafarisayo swali “je, ni kinyume cha sheria kumponya mtu siku ya Sabato?” Mafarisayo hawana jibu. Baada ya kumponya mtu aliyekuwa na ukoma, anawaonya Mafarisayo kwa kushindwa kuonesha huruma, na badala yake kutumia sababu za kisheria.

Mafarisayo hawakuwa na huruma kwa ndugu zao, huyu mtu mwenye ukoma, walikuwa wakijishughulisha na Sabato. Yesu anawauliza kwa mfano alikuwa mwana wao au alikuwa ni punda wao? Yesu anaonesha mioyo baridi ya Mafarisayo, ambao walifikiria kwamba punda ni zaidi ya wana wa Mungu waliokuwa wagonjwa na maskini. 

Kama tukijaribu kumwangalia huyu mtu alieponywa. Ugonjwa ambao ulikuwa ukimtesa ulikuwa ni ukoma, ambapo mwili hutoa maji maji. Sisi kama Mafarisayo huenda tukawa tunaugua ugonjwa kama wa Mafarisayo-pengine si katika hali ya mwili. Hili linakuja pale ambao tunajaza mioyo yetu na ubinafsi na kushindwa kupenda kizuri kwa ajili ya wengine. Ni Yesu mwenyewe anayeweza kuondoa ukame wetu na ubinafsi wetu wa kushindwa kuwapenda wengine kwa uhuru.

Cha muhimu ni kuona mwitikio wetu juu ya wale wanao hitaji msaada wetu, huwa tuna visingizio vingi vya kutoa. Kwa mfano swala la wakimbizi, Baba mtakatifu Fransisko la kuwasahauri parokia na wakristo kuwakaribisha wakimbizi halikupokelewa sana. Swala hili wamelichukulia katika mijadala. Lakini mbaya zaidi hakuna hata tendo lolote la huruma wanalopendekeza wale wanao pinga. 

Leo, tujiulize sisi wenyewe kama nasi tuna mioyo baridi. Je, tupo tayari kuvuka mipaka ya akili zetu na mipaka ya roho zetu kwa aili ya kuwa wakarimu? 

Sala: Bwana Yesu njoo katika moyo wangu, katika hali yangu ya maisha. Njoo zama, katika kazi, kati ya marafiki, katika magumu yangu, wakati wa matatizo, na katika vitu vyangu. Nisaidie mimi niweze kuwa mkarimu kwa ndugu zangu. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com